feet

Injili ya Yohana

Hadithi ya Kweli



Neno Alifanyika Mwili

1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. 3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda. 6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. 9Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. 10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu. 14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. 15 Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” 16Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. 18Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.




Yesu Atakasa Hekalu

12Baada ya hayo, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu, wakakaa huko siku chache. 13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Yesu alipanda kwenda Yerusalemu. 14Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ngʼombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ngʼombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?” 17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.” 18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?” 19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!” 20Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema. 23 Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakaamini katika jina lake. 24Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote. 25Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.



Nikodemo Amwendea Yesu Usiku

1 Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala. 2Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.” 3 Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.” 4Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!” 5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho. 6Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. 7Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili.’ 8Upepo huvuma popote upendapo. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.” 9 Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” 10 Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya? 11Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu. 12Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni? 13Hakuna mtu yeyote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. 14Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”



Yesu Azungumza Na Mwanamke Msamaria

1 Mafarisayo wakasikia kwamba Yesu alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yohana, 2ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. 3Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya. 4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. 5Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yosefu. 6Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. 7 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.” 8(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) 9 Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria. 10 Yesu akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.” 11Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?” 13 Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki, ataona kiu tena. 14Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.” 15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!” 16Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” 17Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. 18Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.” 19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. 20Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.” 21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” 25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Kristo) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.” 26 Yesu akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.” 27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?” 28Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu, 29“Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Kristo?” 30Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Yesu. 31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.” 32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.” 33Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” 34Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. 35Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.” 39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” 40Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. 41Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini. 42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”



Mamlaka Ya Mwana Wa Mungu

19 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo. 20Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa. 21Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma. 24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani. 25Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai. 26Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. 27Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu. 28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. 29Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.



Yesu Ni Mkate Wa Uzima

25 Walipomkuta Yesu ngʼambo ya bahari wakamuuliza, “Rabi, umefika lini huku?” 26 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.” 28Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?” 29 Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.” 30 Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ” 32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” 34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.” 35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.” 41Wayahudi wakaanza kunungʼunika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yosefu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?” 43Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunungʼunikiana ninyi kwa ninyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. 46Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. 47Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48Mimi ni mkate wa uzima. 49Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. 51Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” 52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?” 53 Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.



Yesu Nuru Ya Ulimwengu

12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” 13 Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.” 14 Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. 15Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote. 16Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma. 17Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti. 18Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.” 19 Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.” 20Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.



Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?” 3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. 4Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.” 6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. 7Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu, maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona. 8 Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?” 9Wengine wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.” Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.” 10Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?” 11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!” 12Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?” Akawajibu, “Sijui.”



Mchungaji Mwema

1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwizi na mnyangʼanyi. 2Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. 3Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. 4Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. 5Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” 6Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia. 7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. 9Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele. 11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo. 14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.” 19 Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika. 20Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.” 21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”



Yesu Anatabiri Kifo Chake

20 Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu. 21Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.” 22Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu. 23 Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi. 25Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. 26Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.



Yesu Atabiri Petro Kumkana

31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara. 33 “Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta, na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja. 34 “Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.” 36 Simoni Petro akamuuliza, “Bwana, unakwenda wapi?” Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.” 37 Petro akamuuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.” 38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”



Yesu Awatia Moyo Wanafunzi Wake

1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.” 5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?” 6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. 7Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.” 8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.” 9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba?’ 10Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12Amin, amin nawaambia, yeyote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.

Yesu Aahidi Roho Mtakatifu

15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. 18Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu. 19Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. 20Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu. 21Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” 22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” 23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma. 25“Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. 28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru. “Haya inukeni; twendeni zetu.



Yesu Mzabibu Wa Kweli

1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda. 5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu. 9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.



Yesu Ajiombea Mwenyewe, Wanafunzi Wake, Wote Wamwaminio

1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. 4Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. 5Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo. 6 “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. 7Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, 8kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. 9Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. 11Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia. 13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. 18Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli. 20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi. 24 “Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. 25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”



Kifo Cha Yesu

28 Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.” 29Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. 30Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake. 31 Kwa kuwa ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, hasa kwa kuwa hiyo Sabato ingekuwa Sikukuu. Wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe ili wafe haraka miili iondolewe kwenye misalaba. 32Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Yesu na yule mwingine pia. 33Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake. 34Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni na mara pakatoka damu na maji. 35Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini. 36Kwa maana mambo haya yalitukia ili Maandiko yapate kutimia, yale yasemayo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” 37Tena Andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”



Yesu Awatokea Wanafunzi Wake

19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana. 21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”